26 Juni 2021 - 13:05
Rais wa Afrika Kusini amemtumia ujumbe wa pongezi Rais mteule wa Iran

Rais wa Afrika Kusini amemtumia ujumbe Ayatullah Ebrahim Raeisi akimpongeza kwa kupata ushindi katika uchaguzi wa 13 wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini amempongeza Sayyid Ebrahim Raeisi na akasema anaipongeza pia Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa kuendesha uchaguzi wa amani na wenye mafanikio. Rais Ramaphosa ameongeza kuwa, Afrika Kusini inaitizama Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kama mshirika wake wa kibiashara wa kistratejia katika eneo la Asia Magharibi na iko tayari kushirikiana na serikali ya Iran. 

Ijumaa iliyopita kulifanyika uchaguzi wa 13 wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran uliohudhuriwa na idadi kubwa ya wananchi. Ayatullah Ebrahim Raeisi alipata kura milioni 17 na 926,345 na hivyo kuchaguliwa kuwa Rais wa nane wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. 

Viongozi mbalimbali duniani kuanzia Amerika ya Latini, Russia, Uturuki, Oman, Syria, Pakistan, Iraq, Kuwait, Armenia, Uzbekistan, Arzebaijan, India, Algeria, Nigeria na Imarati pia wametuma jumbe zao wakimpongeza Ayatullah Sayyid Ebrahim Raeisi kwa kupata ushindi katika uchaguzi huo.  

342/